Namna Bora Ya Kusema 'Nisamehe Au Naomba Radhi'.


Ulishawahi kusema kitu kwa rafiki yako kisha ukajisikia vibaya baadae kutokana na kwamba ulichokisema hakikuwa kitu chema? Yawezekana pia ulihitaji kumtaka radhi lakini hukufahamu wapi pa kuanzia.

Tafiti zinaonesha kwamba watu wengi hushindwa kusema 'nisamehe au naomba radhi' kwa sababu wanachanganya kati ya kutenda makosa makusudi na kutenda makosa naturally. Unatakiwa kutambua kwamba hata watu wema husema maneno mabaya kwa rafiki zao.

Habari njema ni kwamba kuomba msamaha ni stadi ambayo unaweza kuijenga ndani yako. Zifuatazo ni hatua nne za kuomba radhi au msamaha pale unapokosea.

1. Kuwa Mkweli.

Hakikisha kila siku unapoomba msamaha, maanisha kile unachokisema. Isiwe kuomba msamaha ilimradi tu! Hata yule anayekusikiliza anatakiwa aelewe msamaha wako kitendo kitakachompa nafasi ya kupokea kile unachokisema kwa kutambua kwamba hata wewe ni binadamu na unajutia kosa ulilomfanyia. Hapa simaanishi kunyenyekea bali kuomba msamaha kwa kumaanisha.

2. Fanya Haraka.

Mara baada ya kugundua umefanya kosa, fanya haraka kuomba msamaha. Maridhiano ya mapema ni tiba tosha ya mahusiano ya muda mrefu. Kadri unavyochelewa kusafisha makosa uliyomfanyia rafiki yako, ndivyo unavyozidi kutishia mahusiano yenu.

3. Fikiri Kabla Ya Kusema.

Uchaguzi wa maneno ya kutumia katika kuomba radhi ni muhimu sana. Maneno sahihi yatamfanya yule unaemwomba msamaha kuona ukweli juu ya unachokisema.

Ni vyema kutumia nafsi yako (mimi) katika kuongea. Kwa mfano badala ya kusema, 'Unaoneka umechukizwa sana na maneno yangu', sema 'Naona hujafurahishwa na kile nilicho kisema'.

Pia epuka kutumia neno 'kama' na badala yake tumia neno 'lakini'. Kwa mfano ukisema, 'samahani sana kama nimekukosea' haina nguvu ya kukili kosa kama ukisema, 'nisamehe kwa kukukosea, lakini sikuwa na lengo...'.

4. Vumilia.

Hata baada ya kuomba msamaha kwa kumaanisha, inawezekana yule unayemwomba msamaha hayuko tayari kukusamehe. Hii ni sawa pia! Msamaha siku zote hautokei mara moja, unachukua muda.

"Chukulia msamaha kama wimbi la maji baharini, mwanzo huonekana ni vigumu kutulia lakini linapofika ufukweni hutulia na kupotea. Ni vyema kuvumilia kutokusamehewa mwanzoni kwa sababu mwishoni hasira zitatulia na msamaha utapatikana"