Uongo Unaouamini Kuhusu Maisha ya Chuo, Tanzania - Part 1

...

Kila mwanafunzi huwa na mtazamo wake kuhusu maisha ya chuo kutokana na kile anachokiona na kukisikia kila wakati maswala ya chuo yanapoongelewa. Makala hii itagusia mambo yasiyo na ukweli katika ujumla wa maisha ya chuo. Experience hii inatolewa na mwanachuo wa chuo kikuu hapa Tanzania akishirikiana na wanafunzi wenzake kutoka kada mbalimbali. Tuanze!

'WANACHUO WANA PESA'

Nikiwa kidato cha sita kuna nyakati nilikuwa natamani sana kufahamu namna maisha yangu ya chuo yatakavyokuwa. Mara kadhaa niliahirisha mipango iliyohitaji pesa nikiwa na imani kwamba nikifika chuoni nitakuwa na pesa ya kutosha kufanikisha yale yote niliyoyapanga. Tulipeana matumaini na wenzangu kwamba chuoni tutakuwa na pesa, tena pesa nyingi.

Idea ya kwamba wanachuo wanapesa sikuitoa usingizini. Ilitokea katika maongezi niliyokuwa nayo na wanafunzi wenzangu na pia mifano ya kaka na dada zetu waliotutangulia. Katika maongezi yetu kuna kosa tulilifanya. Hatukuzingatia kiundani mifano ya wanachuo (kaka na dada zetu) tuliowatazama. Hatukujumuisha vipaji vyao, uwezo wa familia zao wala utashi wa biashara/ujasiriamali walionao.

Nikiwa chuoni.

Nimepata nafasi ya kupima idea ya kwamba wanachuo wana pesa katika kipindi nilichokaa chuoni. Takwimu za ujumla zinaonesha kwamba wanachuo wengi hawana pesa unazozifikiria; Pesa ya kufanya starehe za gharama, pesa ya kufanikisha mipango mikubwa na hata pesa ya kuvaa mavazi na vito vya gharama.

Nitakuwa muongo kama sitokubali kwamba kuna wanachuo wenye pesa ya kutosha. Sasa pesa zaidi wanatoa wapi?

Nimetangulia kusema hapo awali kwamba mambo kama familia wanazotokea, vipaji walivyonavyo na utashi katika ujasiriamali/biashara lazima yazingatiwe. Sababu kubwa ikiwa ni kwamba, hivi ni baadhi ya vitu vinavyowafanya wanachuo wengi kuwa na pesa.

Tumeshaona kwamba wanachuo hawana pesa. Pia tumeona mambo yanayosaidia baadhi ya wanachuo kuwa na pesa ya kutosha. Sasa kabla ya kuingia chuoni huwa tunakosea wapi? Kosa tunalolifanya ni kukubali kupumbwazwa na idea ya kwamba chuoni tutakuwa na pesa bila kufikiria na kuandaa mikakati ya kutengeneza pesa.

Ushauri kwa wanaotarajia kujiunga na vyuo.

Ondoa dhana ya kwamba utakuwa na pesa kirahisi rahisi. Badala yake fikiria kuhusu vyanzo vya mapato utakavyokua navyo (usijumuishe boom kutoka bodi ya mikopo). Kitu kingine, usipange matumizi mengi sana yasiyo na umuhimu. Punguza matumizi, chuo hakuna pesa inayokaa!

Hii ni sehemu ya mwanzo kuhusu mambo ya uongo juu ya maisha ya chuo. Tujulishe hapo kwenye comments kama ungependa kuona mwendelezo wa makala hii. Ni jambo gani lingine unalolisikia sana juu ya maisha ya chuo?

Post a Comment

0 Comments